
Wakati katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akiwa nchini Canada kushughulikia suala la ndege ya Bombardier, waziri mkuu wa nchi hiyo, Justin Trudeau amesema hawezi kuingilia uhuru wa mahakama ambayo anaamini itatenda haki.
Hivi karibuni Rais John Magufuli alisema amemwandikia barua waziri huyo mkuu wa Canada ili kujua hatima ya ndege hiyo.
Hata
hivyo naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta
Nditiye alisema jana kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu
waziri mkuu yupo na wao hawajapata taarifa rasmi.
“Lakini
kingine naomba utambue kuwa katibu mkuu bado yupo Canada, kwa hiyo
mambo mengi mimi sijayapata hadi atakaporudi aje kutu-breaf kilichojiri
huko,” alisema Nditiye.
Akizindua
uwanja wa ndege mjini Bukoba, Novemba 6, Rais Magufuli alisema
amemwandikia barua waziri mkuu wa Canada kumuomba kuachiwa kwa ndege
hiyo na amemtuma mwanasheria mkuu wa Serikali, George Masaju kwenda
nchini humo kushughulikia suala hilo.
Kwenye
barua yake ya majibu ambayo yameripotiwa na gazeti la National Post la
nchini humo, waziri mkuu wa Canada Trudeau amesema hana cha kufanya kwa
kuwa shauri hilo lipo mahakamani.
“Ni
bahati mbaya kwamba suala hili limechelewesha kuwasili kwa ndege hii.
Serikali ya Canada haina uwezo wa kuingilia, ila tuna imani mahakama
itaamua kwa weledi na haki,” amekaririwa akisema Trudeau katika gazeti
hilo.
Ndege
hiyo, Bombardier Q400-8 inashikiliwa kwa amri ya mahakama nchini humo
kutokana na shauri lililopo kati ya Serikali na kampuni ya Stirling
Civil Engineering.
Kampuni
hiyo ilikuwa na mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo
ambao ulivunjika kabla haujakamilika, hivyo ikaamua kukimbilia kwenye
Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa ambako ilishinda kesi. Baada ya
kushinda kampuni hiyo ilipewa kibali cha kukamata mali za Tanzania
katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na
Canada.
Kwa
miezi mitatu sasa, mahakama nchini Canada inaendelea kuishikilia ndege
hiyo iliyonunuliwa kwa Dola 32 milioni za Marekani (zaidi ya Sh70.4
bilioni) kwa niaba ya kampuni ya Stirling inayoidai Serikali Dola 28
milioni (zaidi ya Sh61.6 bilioni) ambazo ni thamani ya mkataba
uliovunjwa pamoja na riba.
Ndege
hiyo ni miongoni mwa zile ambazo Rais Magufuli aliahidi kununua ikiwa
ni mikakati ya kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Awali,
ndege hiyo litarajiwa kuwasili nchini mwezi Julai, lakini hilo
halikufanyika na Agosti 18, akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema ndege
hiyo imekamatwa nchini Canada na inaweza kupigwa mnada kutokana na deni
ambalo Serikali inadaiwa na kampuni hiyo yenye makao yake Montreal,
Canada.
Agosti 19, Serikali ilifanya mkutano na wanahabari kukanusha taarifa hizo, lakini ilikiri kuwapo mgogoro na kampuni hiyo.
Aliyekuwa
kaimu mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa alisema
mgogoro kuhusu ndege hiyo upo na kimsingi umetengenezwa na Watanzania
ambao kwa bahati mbaya wameweka masilahi ya kisiasa na ya binafsi mbele
zaidi ya masilahi ya Taifa.
Alisema
Serikali ilikuwa imeanza majadiliano ya kidiplomasia kwa ajili ya
kulimaliza suala hilo. Kwa sasa, ATCL inamiliki ndege mbili mpya aina ya
bombardier zilizoingia nchini Septemba 2016, na imeagiza ndege nyingine
tatu za aina hiyo na Boeing Dreamliner moja.
Akizungumzia
mafanikio ya miaka miwili ya Rais John Magufuli hivi karibuni msemaji
mkuu wa Serikali, Hassan Abbasi alisema mpaka Juni mwakani ndege zote
zitakuwa zimewasili nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni