
Wanafunzi
watano wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kihinga wilayani
Ngara mkoani Kagera wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa baada ya
kulipukiwa na kitu kinachoaminika kuwa bomu.
Mlipuko huo umetokea leo Jumatano Novemba 8,2017 asubuhi wanafunzi hao walipokuwa wakiingia darasani.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Misheni Rulenge, Goreti Francis amethibitisha kupokewa miili mitatu na majeruhi 20.
Kati ya majeruhi hao, amesema wawili walifariki wakati wakipatiwa matibabu.
“Majeruhi wana majeraha sehemu mbalimbali za mwili, tunafanya kila jitihada kuokoa maisha yao,” amesema Dk Francis.
Akizungumza
kwa simu akiwa eneo la tukio, zaidi ya kilomita 50 kutoka Ngara mjini,
diwani wa Kibogora, Adronis Bulindoli amesema wanafunzi waliofariki wana
umri kati ya miaka minane na tisa.
Amesema
askari polisi kutoka Kituo Kidogo cha Kata ya Bugarama kwa kushirikiana
na maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wa kikosi cha
kulinda mpaka kilichopo Bugarama wanaendelea na uchunguzi eneo la tukio.
Juhudi
za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi na
viongozi wengine wa wilaya kuzungumzia tukio hilo zimeshindikana kwa
kuwa wapo kwenye msafara wa Rais John Magufuli aliye ziarani mkoani
Kagera.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Erick Nkilamachumu amesema kuna
hisia kuwa mmoja kati ya wanafunzi hao alibeba mlipuko unaodaiwa kuwa ni
bomu baada ya kuliokota.
Kata
ya Bugarama ambako Shule ya Msingi Kihinga ipo ni miongoni mwa maeneo
yanayopakana na nchi jirani ya Burundi ambayo imekuwa na mapambano
kuhusu madaraka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni