
KATIKA kuiimarisha safu yao ya ulinzi, Yanga imemshusha nchini beki
Mnigeria, Eisa Mfowoshe aliyemaliza mkataba wa kuichezea Klabu ya Itihad
ya Oman. Ujio wa beki huyo unakamilisha idadi ya wachezaji watatu
waliokuwepo kwenye majaribio ya timu hiyo wengine ni beki Mnigeria,
Henry Okoh na kiungo Fernando Bongyang na Mfowoshe.
Kati ya wachezaji hao mmoja pekee ndiye anatakiwa asajiliwe ili
akamilishe idadi ya wachezaji saba wa kimataifa kati ya sita ambao
tayari wamesajiliwa na Yanga. Championi Ijumaa lilikuwepo kwenye mazoezi
ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam
na kumshuhudia beki huyo akionyesha uzoefu wa kupambana na washambuliaji
wenye uwezo wa juu.
Katika mazoezi hayo, beki huyo mwenye umbile kubwa alionekana akifanya
program zote kwa makini huku akionyesha uhodari wake wa kupiga pasi
zilizonyooka ndefu na fupi kwa wenzake. Wakati mazoezi hayo yakiendelea,
Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina alimpangia washambuliaji wawili,
Donald Ngoma na Amissi Tambwe kwa ajili ya kumpima.
Mnigeria huyo alionyesha uhodari wa kuwadhibiti huku akitumia vema
umbile lake kubwa kuokoa mipira ya juu kwa vichwa na kupanga mabeki
wenzake aliocheza nao akiwemo Kelvin Yondani kama vile wameshacheza
pamoja muda mrefu.
Mara baada ya mazoezi hayo kumalizika, Championi Ijumaa lilizungumza na
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Husseni Nyika kuhusu suala
hilo, alisema:
“Mfowoshe amekuja jana (juzi) na kuanza majaribio na Yanga ili kocha
amuangalie na kama akimshawishi, basi tutamsajili. “Beki huyo ni
mchezaji huru aliyemaliza mkataba wa kuichezea Itihad hivi karibuni kwa
mujibu wa wakala wake.
“Hivyo, wakati akiwa kwenye majaribio, nimezungumza na kocha amjaribu
kwenye mechi dhidi ya Ruvu Shooting tutakayocheza Jumamosi (kesho),”
alisema Nyika. Usajili wa wachezaji wa kigeni utafungwa rasmi Agosti 15,
mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni