
MKAZI wa Kijiji cha Lyapona, Kata ya Kaengesa, Sumbawanga mkoani Rukwa,
Victoria Kalungwizi (67), ameuawa kwa marungu kwa tuhuma za kuiba
mahindi shambani.
Tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji hicho saa 11 jioni kwa
Kalungwizi kupigwa na watu katika sehemu mbalimbali za mwili kwa fimbo
na rungu hadi kufariki dunia.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando,
alisema Jeshi la Polisi mkoani hapa linawasaka watu watatu wanaodaiwa
kumuua mtu huyo.
Alisema chanzo cha mauaji hayo ni tuhuma dhidi ya Kalungwizi kuwa mwizi
wa mahindi. Alisema alishukiwa kuwa ameiba mahindi katika shamba la
Michael Mkombozi.
Kamanda Kyando alisema mbinu waliyotumia watu hao ni kumvizia akiwa
anavuna mahindi katika shamba ambalo si lake. Alisema baada ya kumkuta
walianza kumshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili kwa fimbo
na marungu hadi kumsababishia kifo papo hapo.
Kamanda Kyando alisema baada ya watuhumiwa kutekeleza mauaji hayo,
walitoroka na kukimbilia kusikojulikana na kwamba juhudi za polisi
kuwatafuta zinaendelea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni