Mgodi wa dhahabu wa Acacia Bulyanhulu (BGML) uliopo katika
Halmashauri ya Msalala, mkoa wa Shinyanga jana Jumatano Julai 26,2017
umekabidhi hundi yenye thamani ya Shilingi 460,732,841.08/= kwa ajili ya
ushuru wa Huduma kwa halmashauri ya Msalala.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo,Meneja Mkuu wa Mgodi wa
Bulyanhulu Graham Crew alisema kiasi hicho ni asilimia 67 ya malipo ya
ushuru wa huduma kwa ajili ya kipindi cha miezi sita kuanzia Januari
hadi mwezi Juni mwaka huu ambacho ni asilimia 0.3 ya ukokotoaji wa
ushuru wa huduma wa mgodi huo katika kipindi hicho.
“Jumla ya malipo ya ushuru wa huduma kwa
kipindi cha miezi sita iliyopita ni shilingi za Kitanzania
687,660,956.84/=,ambapo malipo hayo yamegawanywa katika halmashauri
mbili ambazo ni Msalala inayopata asilimia 67 na Nyang’wale iliyopo
mkoani Geita inapata asilimia 33”,alifafanua Crew.
Alisema kutokana na mgawanyo huo,halmashauri ya Msalala imelipwa
shilingi milioni 460 (460,732,841.08/= ) na Nyang’wale shilingi Milioni
226 (226,928,115.76/=.
“Ushuru umepungua kwa kuwa mgodi haujafanya mauzo ya
makinikia ambayo yamezuiwa tangu mwanzoni mwa mwezi machi mwaka huu,
hivyo tunafahamu kuwa tutalipa zaidi tutakapouza makinikia ambayo yapo
yanaendelea kukusanywa mgodini”,aliongeza Crew.
Katika hatua nyingine Crew alisema tangu mwaka 2000 mpaka sasa mgodi
huo umelipa zaidi ya shilingi 10,247,742,957/= za kodi ya ushuru wa
huduma na kampuni ya Acacia ilianza kutoa malipo ya ushuru wa huduma wa
asilimia 0.3 ya mapato ghafi kwa halmashauri husika mwaka 2014.
“Mgodi wetu unaendelea kuwa na matarajio ya
kuchangia kuimarisha sekta ya viwanda kwenye uchimbaji madini katika
halmashauri ya Msalala huku tukiendelea kutekeleza mkakati wa Jamii
Endelevu wa Acacia ulioanzishwa mwaka 2016 kwa kushauriana na wadau
lengo likiwa ni kuchangia maendeleo ya Jamii Endelevu inayonufaika na
kukua kwa uchumi ndani ya jamii ili kujenga mahusiano ya kuaminika”,alisema Crew.
Akipokea hundi hiyo kisha kuikabidhi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Msalala, Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu aliushukuru mgodi wa
Acacia Bulyanhulu kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika
kutoa huduma kwa jami.
“Hiki kiwango cha shilingi milioni 460 tulichopokea ni
kiwango kizuri ingawa kimepungua ulikinganisha na kipindi cha miezi sita
cha Mwezi Juni hadi Desemba 2016,furaha inatujaza kwamba ile shilingi
milioni 300 na zaidi ipo ndani ya Makinikia, yatakapouzwa tutaipata na
tutaendelea kuboresha huduma za kijamii”,alieleza Nkurlu.
Nkurulu alimuomba mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala kuhakikisha
fedha zilizotolewa na mgodi huo zitumike kwa huduma za kijamii kama
zilivyokusudiwa ikiwemo kuboresha huduma za afya na miundombinu.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Simon Berege alisema mapato
waliyopokea kutoka mgodi huo yako chini kwa shilingi milioni 300
ukilinganisha na kipindi kilichopita cha kuanzia Mwezi Julai hadi
Desemba 2016 ambapo mgodi huo ulipokea shilingi milioni 760.
“Sisi tumepokea mapato haya kama tunavyopkea mapato
mengine tunayopata katika halmashauri zetu,mapato haya ni yako chini
ukilinganisha na kipindi kilichopita,tunaambiwa mapato yamepungua
kutokana na Makinikia ambapo sasa yamesimama,hii inaleta changamoto
katika ukusanyaji wa mapato katika halmashauri yetu, tunaamini
mazungumzo baina Acacia na serikali yakiisha halmashauri yetu itapata
mapato mengi Zaidi,” aliongeza Berege.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni