Ijumaa, 30 Juni 2017

Lowassa: Demokrasi imeshaanza na Itaendelea....Hakuna wa kuizuia




Waziri  Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema gurudumu la demokrasia limekwisha kuanza nchini hivyo ni vigumu  kulizuia.

Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,  alirejea  Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam jana baada Juni 27 kuhojiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Alihojiwa  kwa takriban saa nne juu ya kauli alizozitoa kuhusu viongozi wa dini wa kundi la Uamsho na akatakiwa kurudi  jana saa 6.00 mchana.

Akizungumza ofisini kwake Mikocheni, Lowassa alisema baada ya kuitikia wito wa polisi jana, hakuna mengi aliyoambiwa zaidi ya kuelezwa kuwa  upelelezi wa suala hilo unaendelea hivyo arejee  ofisini hapo Julai 13.

Alipoulizwa analichukuliaje suala hilo la kutakiwa kwenda  polisi mara kwa mara  alisema: “Njoo kesho, njoo kesho kutwa ni sehemu ya kazi yao (polisi).

“Kuhusu maoni yangu nitawaambia baada ya kumaliza hili, isionekana naingilia.

“Lakini nieleze jambo moja, demokrasia ikishaanza kuizuia ni taabu sana.

“Unaweza ukapunguza spidi ya gurudumu la demokrasia lakini huwezi kuiondoa, demokrsia imeshaanza, inaendelea, ni vigumu kuizuia.

“La pili, nichukue nafasi hii kuwaomba wanachama wa chama chetu na wananchi na wanaotutakia mema wasiwe na  shaka kila kitu kipo chini ya utaratibu mzuri.

“Tuko sawasawa, tuko sahihi na tunatekeleza kama alivyosema (Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe). Tunatekeleza sera ya chama chetu, wasiogope wawe na amani, watulie,” alisema Lowassa.

Alivyoulizwa kama wakati anatoa kauli kuhusu viongozi hao wa Uamsho labda aliteleza, Lowassa alisema, “I stand by what I said” (naisimamia kauli yangu).

Alisema anaamini alichosema ni sahihi kama alivyoeleza Mbowe na kwamba suala la msingi ni kuachiwa kwa Masheikh wa Uamsho.

Lowassa alisema Chadema  kama chama hakisemi kama viongozi hao wa dini wana makosa ama hawana, ila wamekaa ndani kwa muda mrefu bila kesi zao kusikilizwa.

“Wamekaa vya kutosha, hilo ndilo la msingi tunaloomba… katika hotuba yangu nilisema na kwenye magazeti waliandika vizuri, wale walioko madarakani wana mamlaka.

“Mtu mwenye dhamana ya kuwatoa ni Rais. Nikawaeleza wajipange wakaongee na Rais wamwambie ‘mzee, wenzetu tunaomba waachiliwe’.

“Mwenye madaraka ya mwisho ni Rais, mkiendelea na mahakama miaka minne, nane siyo… kwa hiyo narudia, ni vema wakamuombe Rais awaachilie.

“Sintoshangaa akitekeleza (akawaachia) kwa sababu juzi ametekeleza moja ya uamuzi wetu wa kuunda tume ya kuchunguza madini, tulivyokuwa Kahama tulisema tutaunda tume.

“Waendelee na uchunguzi wao (juu ya kauli yake), lakini narudia, gurudumu la demokrasia likianza kulizuia ni  taabu sana.

“Narudia mwenye mamlaka ya mwisho kuombwa na kushawishiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”alisema Lowassa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni