MWANAMKE mkazi wa Jiji la Dar es Salaam ambaye jina lake halikufahamika,
amesababisha kizaazaa jijini, baada ya kushuka na ungo akiwa uchi wa
mnyama.
Tukio hilo lililoshuhudiwa na kushangaza watu kadhaa waliokuwa na
taharuki, lilitokea juzi karibu na eneo la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
(TAA).
Katika tukio hilo ambalo lilitokea majira ya mchana, mwanamke huyo
alianguka katikati ya barabara katika eneo la Ukonga Banana wilayani
Ilala, akiwa kwenye ungo wake ambao alikuwa ameukalia bila kuvaa nguo.
Mwanamke huyo alikutwa amevaa sidiria yenye rangi nyeupe na kichwa alikuwa amefunga kilemba chenye rangi nyeupe.
Picha za mwanamke huyo zilianza kusambaa katika mitandao mbalimbali ya
kijamii pamoja na video akionekana amekaa katikati ya barabara.
Ungo aliokuwa ameukalia ulikuwa na unga huku akionekana akiongea na
simu. Pia na kwenye masikio yake alionekana amevaa earphones.
Baada ya kugundua yupo katikati ya barabara, alinyanyuka na kwenda
kuokota mizigo yake mingine ambayo ilianguka kandokando ya barabara
hiyo, ukiwamo mkoba na viatu.
Makundi ya watu kadhaa walianza kumfuata huku mwanamke huyo akikimbilia
kwenye kiwanja kilichopo TAA akiwa anajaribu kujificha viongo vyake
visionekane kisha alichukua gauni lililokuwa kwenye begi na kuanza
kulivaa.
Baada ya kuvaa, watu walianza kumzonga na kumzomea wakimuita mchawi na
wengine wakaanza kumtembezea kichapo huku wakimuita mchawi.
“Mwanga, mchawi, muulize anatoka wapi. Kama ni mgonjwa mbona una zana… mchawi, mwanga,” walisikika wakimzonga.
Nipashe ilizungumza na mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaka jina
lake liandikwe gazetini na kueleza kuwa mwanamke huyo anaishi karibu na
Banana.
“Nimeelezwa anapoishi sio mbali, kumbe anajulikana na baadhi ya
wanaomjua wamemshangaa kukutwa na tukio hilo lenye imani za kichawi, cha
ajabu zaidi ameadhirika mchana,” alisema.
Taarifa ambazo hazikuthibitishwa zilidai kuwa mwanamke huyo alichukuliwa
na Polisi kwa lengo la kumuokoa dhidi ya kichapo zaidi kutoka kwa
wananchi waliokuwa na hasira.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, alipoulizwa
jana kuhusiana na tukio hilo, alisema halijaripotiwa katika kituo
chochote cha polisi.