Alhamisi, 1 Februari 2018

JPM asema “Nitachukua hatua, tena mwezi huu wa pili hautaisha”

Rais John Magufuli leo February 1, 2018 katika Maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Mahakama amesema yupo tayari kufanya uteuzi wa majaji wengine ili kukabiliana na changamoto ya upungufu mkubwa wa majaji ambayo inasababisha mrundikano wa mashauri katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Tofauti na hilo Rais Magufuli ametoa wito kwa Mahakama kuendelea kurekebisha dosari ambazo zimekuwa zikiuchafua mhimili huo wa Dola ikiwemo Majaji na Mahakimu kujihusisha na vitendo vya upokeaji wa rushwa na ucheleweshaji wa kesi ambavyo vinasababisha hasara kubwa kwa taifa.
Aidha amempongeza Jaji Mkuu Prof Ibrahim Juma kwa hatua ya kuwafukuza kazi watumishi 112 wa Mahakama wakiwemo Mahakimu 17 waliojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili
Rais Magufuli pia ameeleza kushangazwa na vyombo vingine ambavyo hushirikiana na Mahakama kama vile Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Magereza na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa kutowawajibisha watumishi wake wanaokiuka maadili.
“Mwaka jana nililalamika, sasa mwaka huu sitalalamika, nitachukua hatua, tena mwezi huu wa pili hautaisha, pale ofisini kwangu napokea barua nyingi za malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi, kila kesi upelelezi haujakamilika, ni lazima kuwe na utatuzi wa jambo hili” – Rais Magufuli
“Hivi sasa kuna kesi za Shilingi Bilioni 169.1 na Dola za Marekani Milioni 38.2 zinasubiri tu na nchi inakosa mapato” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.” – Rais Magufuli

Serikali ya Kenya yashtakiwa kwa kufungia vituo vya TV kwenye ‘kuapishwa’ Raila

Mwanaharakati nchini Kenya Okiya Omtatah amefungua mashtaka dhidi ya serikali katika Mahakama Kuu kutokana na uamuzi wake wa kuzima vituo vya televisheni vya Citizen TV, NTV na KTN pamoja na Inooro TV siku ya ‘kujiapisha’ Kiongozi wa Upinzania NASA Raila Odinga.
Omtatah ameeleza kuwa kufungiwa kwa vyombo hivyo vya habari  ni kinyume cha sheria na hakuna sheria yoyote iliyowapa mamlaka ya kutekeleza suala hilo.
Amedai kuwa serikali hiyo lazima izuiwe katika kudharau utawala wa sheria jambo ambalo ni msingi mkuu wa thamani ya taifa na kanuni ya utawala.
Ameongeza kuwa anahitaji mahakama iamuru serikali ilipe fidia vyombo hivyo vya habari vilivyofungwa na kusababishiwa hasara kutokana na jambo hilo.

Wabunge waomba mkataba Mlimani City uchunguzwe

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeliomba Bunge kumuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa mchakato wa mikataba yote ya mradi wa Mlimani City.

Akiwasilisha bungeni leo Februari1, 2018 taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka amesema kamati hiyo imebaini dosari katika mkataba wa uendeshaji wa mradi huo, kusababisha Serikali kukosa mapato.

Miongoni mwa dosari alizozitaja za mradi huo ni kukiukwa kwa sheria ya Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inayotaka ili kibali cha uwekezaji kutolewa lazima mwekezaji alete ushahidi kuwa na mtaji wa kutosha.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilikodisha eneo hilo kwa kampuni ya Mlimani Holding Ltd.

Hivi karibuni PAC ilifanya ziara katika eneo la Mlimani City na kuutaka uongozi wa UDSM kurekebisha mkataba kati yake na kampuni ya Mlimani City Holding Ltd kutokana na mapungufu yaliyojitokeza, huku ikihoji sababu ya mwekezaji huyo kuja na mtaji wa Sh150,000 tu.

Licha ya kutotaja siku, Kaboyoka amesema mara ukaguzi huo utakapokamilika taarifa yake iwasilishwe bungeni.

Mwananchi:

FAO yatoa msaada kwa Tanzania kupambana na viwavi jeshi






Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo wamesaini mkataba wa ushirikiano wenye lengo la kuisaidia Tanzania kujenga uwezo wa kufuatilia na kudhibiti uvamizi wa viwavi jeshi hapa nchini.

Akizungumza katika hafla ya makubaliano hayo mkoani Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,Mhandisi Mathew Mtigumwe, amesema  makubaliano hayo  yamekuja kwa wakati muafaka ambapo Serikali ilikuwa inachukua hatua mbali mbali kukabiliana na tatizo hilo.

Mwakilishi Mkazi wa FAO,Fred Kafeero,amesema  Shirika hilo limekuwa likifanya kazi pamoja na Serikali katika nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Tanzania kudhibiti athari inayosababishwa na viwavi jeshi hivyo.

Kupitia makubaliano hayo,FAO itatoa msaada wa kiutaalamu na kifedha wenye thamani ya Dola za Kimarekani 250,000 ambazo ni zaidi ya Tshs. Milioni 550 kuimarisha ufuatiliaji na kukuza uelewa kuhusu  viwavi jeshi kwa mazao kabla na wakati wa misimu ya kilimo ijayo.

TANZIA: Radio wa Goodlife afariki dunia

Muimbaji kutokea kwenye kundi la Good Lyfe Moses Sekibooga ambaye wengi wanamfahamu Radio kutokea Uganda imeripotiwa amefariki dunia asubuhi ya leo February 1,2018 baada ya kukaa ICU kwa siku kadhaa zilizopita, hii ni baada kuripotiwa kupata ajali ya gari  January 23,2018.




 Msanii huyo ambaye alikuwa akifanya vizuri na mwenzie Weasel,  tangu January 23 mwaka huu hali yake ilikuwa ikiripotiwa kuwa mbaya kufuatia majereha aliyoyapata kutokana na ugomvi wa klabu.
Hapo jana Rais wa Uganda, Yoweri Museven alitoa Milioni 30 kwa ajili ya  matibabu ya msanii huyo, pia kulikuwa na maombi maalumu yalikuwa yameandaliwa kwa ajili ya kumuombea ambayo yalitarajiwa kufanyika February 4 mwaka huu katika kanisa la Light the World.
 


Radio
Muimbaji Radio ameacha pengo kubwa katika kundi la Good Lyfe ambalo liliundwa na yeye mwenyewe pamoja na Weasel ambaye ni mdogo wa muimbaji na legend wa muziki nchini Uganda Joseph Mayanja ambao wengi tunamfahamu kama Jose Chameleon.


Kutoka kushoto ni marehemu Radio akiwa na mwenzake Weasel
Taarifa za kifo cha Radio zinakuja ikiwa ni siku moja imepita toka Rais wa Uganda Yoweri Museveni kuripotiwa kutoa milioni 30 kama mchango kwa ajili ya kuokoa maisha ya staa huyo kwa kugharamia matibabu.
Radio na Weasel wamefanya nyimbo nyingi ambazo zimewahi pia kupata Air time katika TV  na Radio Stations za Tanzania, Don’t Cry ft Wizkid, Zuena na wimbo wa Where You Are waliokuwa wameshirikishwa na Blu 3 na huu uliwafanya wajulikane zaidi Tanzania kutokana na wimbo huo kufanya vizuri.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya February 1


Dar yakosekana katika mikoa 10 iliyofanya vizuri



   Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetoa mpangilio wa ubora wa ufaulu kimikoa wa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2017, huku Dar es Salaam ukikosekana katika mikoa 10 iliyofanya vizuri.

Hata hivyo, mkoa huo umepanda kutoka nafasi ya 18 mwaka juzi, hadi nafasi ya 16 mwaka jana. Katika orodha hiyo mkoa wa Kilimanjaro umepanda kutoka nafasi ya tano mwaka 2016 hadi nafasi ya kwanza mwaka jana.

Mkoa wa Pwani nao umepanda kutoka nafasi ya saba mwaka juzi hadi nafasi ya pili mwaka jana. Katika orodha hiyo Tabora imeshika nafasi ya tatu kutoka nafasi ya 10 mwaka 2016.

Mikoa mingine iliyofuata na nafasi iliyoshika ni Shinyanga (nafasi ya nne kutoka nafasi ya tisa), Mwanza (nafasi ya tano kutoka nafasi ya sita).

Mkoa wa Njombe uliokuwa kwa kwanza mwaka 2016, mwaka jana umeporomoka hadi nafasi ya 15.

Mkoa wa Iringa ulishika nafasi ya pili mwaka 2016, lakini mwaka jana umeporomoka hadi nafasi ya 17 huku Kagera ulioshika nafasi ya tatu, ukishuka hadi nafasi ya tisa.

Mkoa ulioshika mkia katika mpangilio huo ni Kaskazini Unguja uliotoka nafasi ya 29 mwaka juzi hadi nafasi ya 31 mwaka jana, ukifuatiwa na Kusini Unguja ulioshika nafasi ya 30 ambayo pia uliishika mwaka juzi.

Mikoa mitano iliyoshika mkia ni Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na Lindi.   

Jumatano, 31 Januari 2018

TAMISEMI yaagiza Shule ya Sekondari Njombe kuchunguzwa baada ya wanafunzi wote kupata 0






Naibu Waziri Ofisi ya Rais –Tamisemi, Joseph Kakunda ameagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Njombe kufanya uchunguzi wa matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Viziwi Njombe.


Katika matokeo yaliyotangazwa jana Jumanne Januari 30,2018 na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), shule hiyo katika matokeo ya mtihani uliofanyika Oktoba na Novemba mwaka jana watahiniwa wote 21 wamepata daraja sifuri (0).

Naibu Waziri Kakunda ametoa agizo la kufanyika uchunguzi leo Jumatano Januari 31,2018 bungeni alipojibu swali la mbunge wa Buyungu (Chadema), Samson Bilago.

Bilago alitaka kujua ni kwa nini shule za wanafunzi wenye mahitaji maalumu zinafanya vibaya kwenye mitihani.

Akizungumzia hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema walimu waliosoma elimu maalumu watapata ajira bila kikwazo cha kusubiri.

Mkuchika amesema wanasubiri kupelekewa orodha ya walimu hao.

Alikuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini aliyetoa mfano wa shule ya Viziwi Njombe ya wanafunzi wa mahitaji maalumu iliyofanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne akisema ni kutokana na kukosa walimu hao.

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari: Dk. Kigwangalla Aeleza Hatma Ya Wavamizi Katika Hifadhi Ya Bonde La Mto Kilombero

Mzee Majuto baada ya kutembelewa hospitalini na Rais Magufuli


Jumatano ya January 31 2018 Rais John Pombe Magufuli alimtembelea hospitalini muigizaji mzee Majuto, ambaye amelazwa hospitali ya Tumaini Upanga jijini Dar es Salaam, lengo likiwa kumjulia hali, Mzee Majuto anasumbuliwa na tatizo la tezi dume.

Maamuzi ya serikali ya Kenya kwa vituo vya TV vilivyoonesha ‘kuapishwa’ kwa Odinga

Waziri wa Mambo ya Ndani Kenya Fred Matiang’i amesema kuwa vyombo vitatu vya habari ambavyo vilifungwa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo jana baada ya kurusha matangazo ya ‘kuapishwa’ kwa Kiongozi wa Upinzani NASA Raila Odinga, vitaendelea kufungwa.
Ameeleza kuwa vyombo hivyo ambavyo ni Citizen TV, KTN na NTV vitaendelea kuwa vimefungwa mpaka uchunguzi utakapofanyika kuhusiana na kile alichokiita ‘uvunjwaji wa usalama uliopindukia’ na kuwa umekamilika.
“Serikali ilifahamu na bado inafahamu jukumu la vyombo hivyo vya habari vilivyoshiriki katika uendelezaji wa jambo lililo kinyume na sheria. ushiriki wao ungeweza kusababisha vifo vya maelfu ya Wakenya wasio na hatia” – Fred Matiang’i

Ilipofikia kesi ya Mbunge Lijualikali na Suzan Kiwanga Mahakamani leo

Wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Morogoro, Peter Lijualikali na Susan Kiwanga pamoja na wafuasi wa chama hicho wapatao 55 wamefika katika Mahakama ya Hakimu mkazi wa mkoa huo kwa ajili ya kesi ya jinai namba 296 ya mwaka 2017 inayowakabili.
Wabunge hao pamoja na wafuasi wao wanatuhumiwa kwa makosa nane ikiwemo ya kuanzisha vurugu na kuchoma mali za umma katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani Novemba 26, mwaka jana ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 27 mwaka huu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mawikili wa utetezi wamesema, walikubaliana kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo baada ya mwezi kwa mujibu wa sheria licha ya kwamba haitaweza kusikilizwa kutokana na Mahakama Kuu kuhamia katika mahakama hiyo kwaajili ya kusikiliza kesi zinazowahusu.
Amesema, waliomba tarehe hiyo kwa lengo la kutajwa tu ili siku hiyo wapange tarehe ya kuanza kusikilizwa kwaajili ya kuwawezesha wateja wao waweze kumaliza kesi hiyo na kurejea katika majukumu yao. Wameiomba mahakama hiyo kutenda haki kwa kusikiliza kesi hiyo kwa haki ili kuondoa dhana iliyopo ya kwamba kesi hiyo inaendeshwa kisiasa

Aubameyang katua Arsenal Giroud kaondoka nae



kadhaa wa baada ya club ya Arsenal kuthibitisha kumsajili staa wa soka wa kimataifa wa Gabon aliyekuwa anaichezea Borussia Dortmund ya Ujerumani Pierre-Emerick Aubameyang, mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa aliyekuwa Arsenal Oliver Giroud ameondoka nae.

Giroud ameondoka Arsenal na kwenda kujiunga na club ya Chelsea kwa ada ya uhamisho wa pound milioni 18 lakini Chelsea nao wamemtoa kwa mkopo mchezaji Batshuayi kwenda Borussia Dortmund ya Ujerumani.
Oliver Giroud ameondoka Arsenal na kujiunga na Chelsea baada ya kudumu ndani ya club ya Arsenal kwa miaka sita alipojiunga nayo 2012 akitokea Montpellier.