na deus liganga
Mkoa wa Morogoro ni Mkoa wa pili kwa
ukubwa nchini ukitanguliwa na Mkoa wa Tabora. Mkoa una eneo la kilometa za
mraba 73,039. Eneo hili ni sawa na asilimia 7.7 ya eneo lote la Tanzania Bara,
kati ya eneo hili Km2 2,240 ni eneo la maji. Mkoa umepakana na Mikoa ya Pwani
na Lindi kwa upande wa Mashariki, Manyara na Tanga kwa upande wa Kaskazini na
kwa upande wa Magharibi umepakana na Mikoa ya Dodoma na Iringa na Upande wa
Kusini unapakana na Mkoa wa Ruvuma na Njombe.
kwa kifupi tu Mkoa wa Morogoro ulianza rasmi mwaka
1962 ukiwa na Wilaya tatu ambazo ni Morogoro Kilosa na Ulanga. Ni Mkoa wa pili
kwa ukubwa hapa nchini kwa sasa ukitanguliwa na Mkoa wa Tabora.
IDADI YA WILAYA KATIKA MKOA WA MOROGORO
Mkoa wa Morogoro kiutawala
umegawanyika katika Wilaya saba ambazo ni Wilaya za Morogoro, Mvomero, Kilosa,
Kilombero, Ulanga, Malinyi na Gairo.
bwawa la ngapemba kata ya utengule wilaya ya kilombero picha na deus liganga mwandishi
hakika mkoa huu umejaliwa kuwa na vivutio vingi ambavyo kama vitaendelezwa vizuri ,vinaweza kuinua nchi na mkoa husika, moja wapo ya tunu ambazo mkoa huu imejaliwa ni bonde la mto kilombero
Bonde la Mto Kilombero
ambalo lipo katika wilaya za Ulanga na Kilombero, mkoani Morogoro, lilikuwa
moja ya vivutio vikubwa vya sayari yetu hii. Vivutio vyake vilivuma hadi nje ya
nchi kiasi hata cha kusababisha bonde hilo kuingizwa katika orodha ya maeneo ya
dunia yanayolindwa na Ramsar; yaani ule mkataba wa kimataifa unaolenga
kuhifadhi ardhioevu (wetlands) muhimu duniani.
Sifa zake zilikuwa nyingi: Bonde la Kilombero lilikuwa na mtandao wa mito zaidi ya 79 iliyokuwa ikititirisha maji misimu yote ya mwaka ambapo mito ya Luhuji, Mnyera, Furua, Mpanga, Kihanzi, Luipa, na Ruaha Mkuu huungana na Mto Kilombero na kuwa Mto Rufiji.
Si hivyo tu. Bonde la Mto Kilombero lilikuwa ndiyo makazi ya asilimia 75 ya wanyamapori aina ya Sheshe duniani. Aidha, ndiko pekee duniani vilikopatikana baadhi ya viumbe hai duniani kama vile vyura wa njano wa Kihansi au Mbega Wekundu wa Udzungwa.
Mbali ya hayo, Bonde la Mto Kilombero lilikuwa ndilo pekee nchini ambako unaweza kupata aina nyingi zaidi za samaki (takriban 40) kuanzia kambale na perege wanaopatikana sehemu nyingi nchini hadi Kapatwa, Ndungu, Ningu nk ambao hupatikana sehemu chache tu.
Hivyo ndivyo Bonde la Kilombero lilivyokuwa angalau miaka 30 iliyopita;
pichani ni mwandishi wa makala hii deus liganga alipokuwa safarini kuelekea katika bwawa la ngapemba kata ya utengule kilombero mwezi june.
Kwa mfano, taarifa zilizopatikana kutoka Idara ya Maliasili ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, mjini Ifakara, zinaonyesha kwamba mito ambayo hutiririsha maji mwaka mzima sasa imebakia 39 tu katika bonde zima kutoka idadi ya mwanzo ya mito 79.
Aina za samaki nazo zimepungua kutoka 40 za mwanzo hadi 20 za sasa. Angalau wenyeji katika vijiji kadhaa vya wilaya ya Kilombero ambapo mwandishi wa makala nimevitembelea wamethibitisha kwamba samaki aina ya Kapatwa ametoweka kabisa katika bonde hilo. Aina nyingine ya samaki ambao wamepungua sana na wapo katika hatari ya kutoweka kabisa ni Ndungu, Mjongwa, Ningu na Mdelwa (golden fish).
Hata kwa wanyamapori hadithi ni hiyo hiyo. Wenyeji wa vijiji vya wilaya hiyo walieleza kwamba sasa ni taabu mno kumuona mnyama anayeitwa Mbega katika mapori yao wakati ambapo zamani walikuwa wengi mno.
Je nini kimetokea? Ilikuaje Bonde la Kilombero ambalo lilikuwa na mito 79 inayotiririsha maji mwaka mzima libakie na mito ya namna hiyo 39 tu? Ilikuaje mpaka wanyama kama Mbega na samaki kama Kapatwa sasa wawe ni historia katika Bonde la Mto Kilombero?
Kuna mambo mengi yanayoweza kutajwa yaliyosababisha hali hiyo hasi, lakini yote yanaweza kujumuishwa katika jambo moja kubwa; nalo ni uharibifu wa mazingira unaoendelea kwa kasi katika bonde hilo - uharibifu ambao athari zake zimekuwa ni maradufu kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi (climate change) yanayoisumbua dunia nzima.
Japo Bonde la Mto Kilombero liliorodheshwa rasmi kuwa eneo la Ramsar (Ramsar site) tangu Aprili 26, 2002 na kuanzia muda huo Ubelgiji imekuwa ikifadhili mradi wa Ramsar kwenye bonde hilo kupitia Halmashauri za wilaya ya Ulanga [sasa wilaya mpya ya malinyi ]na Kilombero, bado kasi ya uharibifu wa mazingira katika bonde hilo inafifisha mafanikio ya mradi huo.
Lakini pengine kinachokatisha tamaa zaidi ni kwamba wakati mradi wa Ramsar ukijaribu kuliokoa bonde hilo, Serikali imekaribisha ‘tatizo jipya’ katika bonde hilo; tatizo ambalo, kwa sasa, ndilo linalochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira katika bonde hilo. ‘Tatizo jipya’ linalozungumziwa hapa ni uvamizi wa wafugaji wa Kisukuma katika Bonde la Mto Kilombero.
mwandishi alijionea katika ziara hiyo namna vyanzo mbalimbali vya maji vilivyoharibiwa na wafugaji hao wa Kisukuma ambao wamevamia bonde hilo na maelfu ya mifugo yao wakitokea Ihefu (Mbarali) ambako walitimuliwa na serikali mwaka 2006 baada ya kuiharibu pia ardhioevu hiyo.
Wafugaji hao wa Kisukuma ambao kwa desturi na tabia zao chafu si rafiki wa mazingira, wamekata miti katika mapori mengi na kuweka maskani yao katika vyanzo vingi vya maji katika Bonde la Kilombero.
Kwa hakika, wamekuwa ndiyo kero kubwa katika vijiji vingi ambavyo niliweza kutembelea wakati wa ziara hiyo.
“Hebu wafikishieni salamu wakubwa serikalini huko Dar es Salaam: Wasipochukua hatua ya kuwafukuza wafugaji hawa wa Kisukuma, vyanzo vyote vya maji vitatoweka, na hata Mto Kilombero hautakuwa na maji mengi.
Katika vijiji vingine vya Njage, Mngeta, Mchombe, Merera na hata mji mdogo wa Mlimba, kidole cha uharibifu wa mazingira kilielekezwa kwa hao hao wafugaji wa Kisukuma waliotimuliwa kutoka Mbarali (Ihefu).
Katika kijiji cha Njagi, mjumbe wa Serikali ya kijiji, Abdallah Iporah, anakiri kwamba mabadiliko ya tabianchi yamechangia mno kuvisambaratisha vivutio vya Bonde la Kilombero. “Zamani hapa tulikuwa tukipata mvua karibu kila mwezi, lakini sasa hatuna tena uhakika wa mvua. Kuanzia Mei hatujapata mvua hata mara moja. Tulipanda mahindi lakini yamekauka.”
Lakini pamoja na mabadiliko ya tabianchi, mzee huyo bado anaelekeza kidole chake kwa wafugaji wa Kisukuma kwamba wanachangia zaidi katika kuyafanya maisha yao wote kuwa magumu zaidi.
“Wamevamia maeneo yetu kwa mamia. Kwanza anakuja mmoja na anawasilisha maombi ya kuishi kijijini kwa serikali ya kijiji. Akishakubaliwa anakaa kama wiki moja tu na kuondoka kwenda kuchukua ng’ombe wake kibao. Baada ya muda anamwita mwenzake na mwenzake naye anamwita mwenzake. Na wote hao kila mmoja ana wake si chini ya wanne na watoto kibao na ng’ombe kibao. Baada ya muda wanavivamia vyanzo vya maji na mifugo yao, na hakuna tena wa kuwaambia “ondokeni”. Wanakuwa wakali na wako tayari kuua”, anasema mzee huyo.
Uharibifu huo wa mazingira na vyanzo vya maji unaofanywa na wafugaji hao wa Kisukuma ukichangiwa na mabadiliko ya tabianchi, vimeyafanya maisha ya wanavijiji wengi katika Bonde la Kilombero yawe magumu zaidi.
Otwin Mafui ni Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Merera. Anasema: “Zamani samaki walikuwa bwerere. Kikombe kikubwa kilichojazwa samaki wadogo wabichi ulikuwa ukikipata kwa Sh. 200 tu, lakini sasa kwa kiasi hicho hicho cha pesa unapata samaki mmoja tu. Mwaka 2003/2004 kambale mmoja alikuwa anauzwa Sh. 1,000, sasa ni kati ya Sh. 5,000 na Sh. 10,000.”
Kwa nini samaki wamepungua katika kijiji chake? Jibu lake ni kwamba maeneo mengi ya ardhioevu ambako walikuwa wakipatikana kwa wingi yamekauka kabisa, na pia samaki wamekimbia katika baadhi ya mito kwa sababu ya kupungua vina vya maji na kuharibiwa kwa maeneo ya mazalio yao.
Mvuvi Alex Ndalala alifikia hatua ya kuutajia haraka haraka ujumbe huo wa majina ya mito ya maeneo yao ambayo imekauka. “Mto Mkusi umekauka, Mto Mpakaka umekauka, Mto Nagakuru umekauka, Mto Mkula umekauka... na bwawa la asili la Mhoma nalo ikifika mwezi wa nane tu limekauka. Sasa unadhani hizo samaki zitatoka wapi?”, anauliza.
pia mwandishi alitembelea kata ya Utengule ,jimbo la mlimba na kujionea wenyewe jinsi bwawa kubwa la enzi na enzi la Ngapemba lilivyoathiriwa na climate change na wafugaji hao wa Kisukuma.
Bwawa hilo lililokuwa na ukubwa wa eka za mraba 1,000 na lililokuwa na hekaheka nyingi za uvuvi, sasa limenyauka na kusinyaa na kubakia eka chache tu za mraba.
Zamani bwawa hilo lilikuwa likichukuliwa kuwa ni takatifu (sacred) kwa imani za makabila ya asili ya maeneo hayo. Ndani ya bwawa hilo kulikuwa na msitu mdogo ambako wanavijiji walikwenda kwa ajili ya kufanya matambiko yao.
Kwa sababu hiyo, ilijengwa imani kwamba mtu yeyote ambaye angetenda chochote dhidi ya ustawi wa bwawa hilo kama vile kuvua samaki wachanga na kuwatupa au kuziba mikondo ya maji yanayoingia katika bwawa hilo, angepotezwa kabisa duniani bila mwili wake kuonekana! Kuna hata simulizi za watu inaoaminika walipotea kwa kufanya vitendo kinyume na ustawi wa bwawa hilo!
Imani hizo za kale, kwa kiasi kikubwa, zilichangia kulitunza bwawa hilo miaka hadi miaka. Lakini hali ilianza kubadilika kwa kasi mwaka 2006 wakati wafugaji hao wa Kisukuma waliofukuzwa kutoka Ihefu walipovamia maeneo jirani na bwawa hilo.
Kwa wafugaji hao wa Kisukuma, ‘vitisho’ vya imani hizo za kale havikuwazuia kuyavamia maeneo ya pembeni ya Bwawa la Ngapemba yaliyokuwa na nyasi mbichi kulisha ng’ombe zao. Na huo ndio ukawa mwanzo wa kusinyaa na kukauka kwa Bwawa la Ngapemba.
Huhitaji kuwa mtaalamu wa mazingira kutabiri kwamba bwawa hilo ambalo maelfu ya wanavijiji wa Bonde la Kilombero walikuwa wakinufaika nalo sasa lipo “ICU”, na muda si mrefu litatoweka kabisa katika uso wa dunia.
Pengine swali la kujiuliuza ni hili: Je; Serikali inafanya nini kuhusu wavamizi hao wa wafugaji wa Kisukuma katika Bonde la Mto Kilombero?
Wapo wadau wa mazingira wanaoamini kuwa hivyo ndivyo itakavyokuwa, lakini wapo wengine wanaoamini kwamba hilo halitatokea; na hao wanadai kwamba wafugaji hao wa Kisukuma wana ka-uwezo ‘fulani’ ka kuwaweka mfukoni watendaji wa Serikali na kuwafanya kuendelea kusitasita kuchukua hatua za kuwatimua.
muda unayoyoma kwa Bonde la
Kilombero. Kwa hali ambayo blog hii ilijionea katika ziara ya bonde hilo, hakutabaki
kivutio chochote cha maana katika kipindi cha miaka 10 ijayo kama hatua ya
kuwafukuza wafugaji hao itacheleweshwa na uhifadhi wa mazingira kuendelezwa
makala hii imeandikwa na deus liganga ambaye ni mwandishi wa habari kitaaluma ,kwa msaada wa chama cha waandishi wa habari za mazingira JET mawasiliano 0684495100,0659944423 ,deusliganga@yahooo.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni