Ijumaa, 8 Juni 2018

Yanga yamwandikia barua Manji


MAANDALIZI ya Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Yanga yamekamilika kwa asilimia kubwa huku ikipanga kutoa mwaliko maalum kwa aliyekuwa mwenyekiti na mfadhili wao Yusuf Manji.

Yanga imepanga kufanya mkutano huo Jumapili hii kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi, Masaki jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa alisema tofauti na Manji wamepanga kuwaandikia barua ya mwaliko viongozi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

“Baadhi ya ajenda zitakazowasilishwa kwenye mkutano huo ni pamoja na ushiriki wa Yanga katika michuano ya kimataifa ikiwemo hatua tuliyofikia kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho, Mapato na Matumizi, bila ya kusahau mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji.

“Pia, suala la uchaguzi wa kujaza nafasi zilizokuwa wazi huenda likawasilishwa kupitia mengineyo ingawa kuna uwezekano mkubwa kwa ajenda hiyo kuondolewa ili kuwapa nafasi wanachama kujadili masuala muhimu,” alisema Mkwasa ambaye amewahi kuwa kocha wa Yanga.

Manji ni kati ya wanachama wenye nguvu kubwa kwenye timu hiyo ya Jangwani na baadhi wanaamini kuwa anaweza kuwasaidia kutoka kwenye taabu walizonazo sasa za kiuchumi kama atakubali kurejea.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni