Mshambuliaji hatari wa Simba, Emmanuel Okwi.
MSHAMBULIAJI hatari wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda amefunguka
kuwa anazihofia timu ambazo watakutana nazo kwenye mechi zijazo kwa
sababu timu hizo watawapania kwa ajili ya kutaka kuvunja rekodi yao ya
kutokufungwa.
Kinara huyo wa mabao ligi kuu amewaongoza Simba kutwaa ubingwa kwa
msimu huu lakini pia wakiwa hawajafungwa kwenye mechi zao 28 ambazo
wamezicheza hadi sasa huku wakiwa wamebakisha michezo miwili pekee.
Simba inayonolewa na Mfaransa, Pierre Lechantre imebakisha michezo dhidi
ya Kagera Sugar ambao wataucheza kwenye Uwanja wa Taifa, Mei 20, kabla
ya kwenda kuhitimisha msimu wao ugenini kwa kucheza na Majimaji ya
Songea.
akizungumza na Championi Jumatano, Okwi aliyefunga mabao 20 kwenye ligi
amesema wanatakiwa kupambana zaidi kwenye mechi hizo mbili kwa ajili ya
kutafuta matokeo mazuri kwa sababu wapinzani wao wataingia uwanjani
wakiwa na wazo moja la kuwatibulia rekodi yao ya kutokufungwa hadi
sasa.
“Kwetu bado hatujamaliza ligi tunatakiwa kupambana zaidi kuhakikisha
kwamba tunashinda kwenye mechi hizi ambazo zimebakia, ni muhimu
kuendelea kutafuta matokeo mazuri kwa ajili ya kuitunza rekodi ya
kutofungwa kwa msimu huu.
“Najua wapinzani wetu wanaofuata Kagera na Majimaji watakuja uwanjani
kwa kupania mechi na kucheza kwa nguvu ili tu waweze kututibulia rekodi
yetu ya kutofungwa, hivyo itatulazimu sisi kupambana kushinda mechi
hizo,” alisema Okwi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni