Jumapili, 27 Mei 2018

Chadema kumuaga Mbunge wao kesho Karimjee


Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, kimetoa taarifa ya ratiba ya kuaga mwili wa Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago ambaye pia alikuwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama na Mwenyekiti wa Chama Kanda ya Magharibi yenye Mikoa ya Kigoma,Katavi na Tabora.

Kwa upande wa Bunge Marehemu alikuwa Naibu  Waziri Kivuli katika wizara ya  Elimu na Mafunzo.

Taarifa hiyo inasema baada ya kikao baina ya familia na Viongozi wakuu wa Chama kilichofanyika leo tarehe 27 Mei,2018 ratiba iliyokubaliwa ni kama ifuatavyo;

Jumatatu tarehe 28 Mei 2018 ni ibada fupi na kuuaga mwili katika viwanja vya Karemjee Dar kuanzia saa sita kamili mchana na mwili kupelekwa uwanja wa ndege, Dar es Salaam.

Tarehe 29 Mei siku ya Jumanne asubuhi mwili utapokelewa uwanja wa ndege, Dodoma na kupelekwa Bungeni ambapo  Wabunge watauaga mwili katika viwanja vya Bunge Dodoma. Baada ya hapo mwili utasafirishwa kwa ndege kuelekea Kibondo.

Tarehe 30 Mei siku ya jumatano wananchi wa Jimbo la Buyungu watapata fursa ya kuuaga mwili katika eneo  litakalotangazwa baadae.

Alhamisi tarehe 31 Mei, ndio siku ya Mazishi rasmi ambayo yatafanyika Nyumbani kwa Marehemu huko Wilayani Kakonko, Kigoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni