Ijumaa, 16 Machi 2018

TFF wajibu hoja za Michael Wambura

Shirikisho la soka nchini TFF limejibu tuhuma zilizotolewa na makamu wa rais wa shirikisho hilo Michael Richard Wambura, baada ya hukumu ya kufungiwa maisha kutangazwa dhidi yake na kamati ya maadili inayoongozwa na mwenyekiti Hamidu Mbwezeleni.

Wambura alizungumza na waandishi wa habari kupinga hukumu iliyotolewa dhidi yake, huku akiweka wazi  baadhi ya mambo ambayo anaamini yamekua mzizi wa yeye kufanyia figisu hadi kuingizwa hatiani.

Mdau huyo wa soka alidai kuwa, kuna mambo mengi yanaendelea ndani ya TFF likiwepo suala la ubadhilifu wa fedha, ambao umekua kinyume na utaratibu, jambo ambalo aliahidi kulitafutia siku la kulianika hadharani kupitia vyombo vya habari.

TFF imejibu tuhuma hizo kwa kutoa ufafanuzi wa kina katika kila kipengele ambacho kilizungumzwa na Wambura alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.


1.Matumizi mabaya ya fedha za TFF
JIBU : Wambura kama Mwenyekiti wa kamati ya fedha amehudhuria vikao zaidi ya 4 vya kamati na hajawahi kulalamika kokote mpaka amefungiwa.

Bajeti ya TFF iliyopitishwa Dodoma kwa Mwaka Mzima ni Bilioni 8.6 hivyo matumizi anayosema ya Bilioni 3 kwa miezi 7 yanaonyesha jinsi gani TFF inavyopambana na changamoto za kifedha hivyo kuhakikisha inapunguza matumizi.

Mapato yaliyopatikana kwa miezi Saba (7) iliyopita yalitumika katika maeneo yafuatayo :

Timu ya Taifa Taifa stars(Fifa dates),Kilimanjaro Stars  (Challange Cup),Kambi kwa Timu ya Taifa Under23, Kambi U20, U16, Wanawake U20, Ligi za Wanawake, Kombe la Shirikisho la Azam, kozi za makocha,kozi za waamuzi za nje na ndani, vikao vya kamati ya utendaji na  kamati ndogo ndogo, mishahara ya watumishi wa TFF na makocha wa timu za Taifa, kulipa madeni tuliyoyakuta na kuidhinishwa na kamati ya fedha, kozi za Grassroots na Live Your Goal na soka la Ufukweni

2.Ajira za TFF watu kupewa kwa kujuana.
JIBU : TFF haijawahi kuajiri nafasi yoyote ile zaidi ya Wakurugenzi 3 na meneja 1 tofauti na uongo unaozungumzwa,Wakurugenzi walioajiriwa ni Mkurugenzi wa Fedha,Mkurugenzi wa Mashindano,Mkurugenzi wa sheria na Wanachama na Meneja Masoko,katika kupunguza matumizi ya fedha Taasisi imebaki na Wafanyakazi 21 kutoka 44 wa awali waliokutwa na Ndugu Karia.

3.Kumteua Wilfred Kidao kuwa kaimu Katibu Mkuu wa TFF.
JIBU : Kaimu Katibu Mkuu alikaimishwa na Kamati ya Utendaji na yeye Wambura akiwa mmoja wa waliompitisha.

4.Mipira 100 kila mkoa kwamba kuna watu wamepiga fedha za TFF.
JIBU : TFF chini ya Rais wa TFF aliyekuwepo madarakani Ndugu Wallace Karia haijawahi kununua mipira,mipira iliyotolewa ilinunuliwa na uongozi uliopita ilichofanya TFF ni kuigawa kama ilivyofanya.

5.Kuwa na wafanyakazi wawili kwenye nafasi moja.
JIBU : TFF haijawahi kuajiri mfanyakazi zaidi ya mmoja kwenye nafasi moja,wengi waliokuwepo kwenye Shirikisho kwa sasa wanajitolea akiwemo Afisa Habari.

6.Suala la Waamuzi kuondolewa kuchezesha ligi kuu.
JIBU : Ili kuongeza ubora wa uchezeshaji TFF ikaamua kuchaguwa waamuzi wa juu(Elite) tofauti na awali ambako kulikuwa na idadi kubwa mchanganyiko ya waamuzi.

7.Kaimu Katibu kutuma majina ya Makamishina.
JIBU : Jina la Michael Wambura na Ahmed Mgoyi ndio yaliyopelekwa kama utaratibu unavyotaka ya kujaza kwenye fomu moja pekee na TFF haikuwahi kubadilisha wala kukata jina la mtu yeyote.

8.TFF ya sasa mpaka uwe na urafiki na watu 3 Karia, Mgoyi, na Nyamlani.
JIBU : TFF haiendeshwi kwa urafiki bali kwa utaratibu wenye kufuata kanuni.

Kikao kilichotoa maamuzi ni Kamati inayojitegemea (Independent) sio rahisi kuingiliwa kwa kuwa hata Rais wa TFF hawezi kuiingilia

Kumekuwa na upotoshaji mkubwa unaoenezwa kwa maslahi binafsi,ni vyema watu wakajikita kwenye kujibu tuhuma zao bila kuhusisha uongo na vitu visivyo vya kweli kwa Taasisi ambayo kwasasa ipo makini kwenye kuhakikisha kila kitu kinafuata utaratibu ikiwemo masuala ya kifedha pamoja na mambo mengine.

Imetolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano TFF

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni