Akizungumza na MCL Digital leo Februari 12,2018 Mwaipopo amethibitisha uteuzi huo.
Taarifa iliyotolewa kwa wafanyakazi na ofisa mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, Peter Geleta imesema uteuzi huo unaanza mara moja.
Geleta amesema Mwaipopo atakuwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni zote zilizopo Tanzania na ataendelea kufanya kazi Dar es Salaam.
Mwaipopo, ni mhandisi migodi mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika sekta ya uchimbaji madini.
Amewahi kushika nyadhifa za uongozi wa juu akisimamia masuala ya uendeshaji na ya shirika katika kampuni kadhaa zikiwamo AngloGold Ashanti, Mantra, African Barrick Gold na Acacia.
Soma: Mtikisiko Acacia
"Uongozi wake, ujuzi wake na uzoefu mkubwa alionao katika sekta ya madini unamfanya kuwa ni chaguo bora kwa ajili ya kuimarisha na kuifanya biashara ya uchimbaji madini Tanzania kuwa thabiti," imesema taarifa hiyo.
Mwaipopo ana shahada ya sayansi katika uhandisi migodi kutoka Chuo Kikuu cha Zambia. Pia, ana shahada ya uzamili ya uhandisi migodi aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Madini cha Camborne nchini Uingereza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni