MWANAMKE mmoja, raia wa Japan amefichua picha zinazomwonyesha
alivyokonda na kubaki na uzito wa kilo 16.8 tu wakati anaokolewa kutoka
katika mikono ya babu yake ambaye aliamua kumnyima chakula.
Mkazi huyo wa Kyoto, Japan, alikuwa akinyimwa chakula na babu yake
katili na aliyekuwa akimpiga kila wakati tangu alipokuwa mdogo hadi
alipookolewa na watu miaka kumi iliyopita kutoka katika janga hilo
lililomwacha akiwa na ngozi iliyofunika mifupa na mbavu zilizochongoka.
Akisimulia mkasa huo, mwanamke huyo ambaye jina lake limefichwa,
japokuwa picha zake zipo, amesema kibabu hicho kilimpiga marufuku kula
bila sababu yoyote, kikawa kinamtukana na kumpiga mateke tumboni ili
kumlazimisha akitapike chakula ambacho alikuwa akila kwa kujificha
wakati kibabu hicho hakipo.
Katika ujumbe alioutuma kwenye mitandao ya kijamii sambamba na picha
hizo, amewataka watu wanaopitia mateso kama hayo, kutafuta msaada haraka
kabla mambo hayajaharibika.
Anasema aliokoka kutoka katika mkasa huo wa kutisha “zikiwa zimebaki dakika kumi tu kabla ya kufikia kifo”.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii walipodai kwamba amefoji picha hizo,
mwanamke huyo alituma picha kadhaa alizopigwa akiwa hospitali ambazo
zinaonyesha majeraha kwenye kifua na shingo yake yaliyosababishwa na
mateso ya kibabu hicho.
Hata hivyo, mwanamke huyo hajafichua hatua zilizochukuliwa dhidi ya babu
yake huyo na kwamba watu wengine wa familia yake walikuwa wapi wakati
hayo yanatendeka.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni