
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa matumizi ya pori tengefu la Loliondo ambao umedumu kwa takriban miaka 26.
Hatma
hiyo imefikiwa jana (Jumatano, Desemba 6, 2017) kwenye kikao
kilichoitishwa na Waziri Mkuu ofisini kwake Mlimwa, Manispaa ya Dodoma
ili kutoa mrejesho uliofikiwa na Serikali kuhusu utatuzi wa mgogoro huo
baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi.
Waziri
Mkuu alisema Serikali imekubali mapendekezo ya kuunda chombo maalum
kitakachosimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya
Serengeti na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya
wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji.
“Baada
ya kupitia mifumo mbalimbali, timu ya wataalam ilipendekeza kuwa
utumike mfumo maalum utakaounda chombo maalum, kwa kuwa una maslahi
mapana kwa pande zote husika na unalenga kuleta amani na kufikia lengo
la kuwa na uhifadhi endelevu katika eneo la Loliondo,” alisema.
Waziri
Mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili iandae muswada wa kutunga sheria
mahsusi ya kuwa na chombo maalum au mamlaka ya kusimamia eneo la
Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti pamoja na kulinda
mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo
vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi muhimu zenye maliasili na
rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wenyewe na Taifa kwa ujumla.
“Sheria
itakayotungwa ihakikishe inawekewa masharti yanayozingatia maslahi ya
jamii iliyopo katika eneo la Loliondo, mila zao na desturi zao pamoja na
mahusiano yao na matumizi ya ardhi,” alisisitiza Waziri Mkuu na
kushangiliwa na wajumbe zaidi ya 60 waliohudhuria kikao hicho.
Vilevile,
Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae waraka
maalum utakaowasilishwa Serikalini kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu
umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo la Loliondo.
Alisema
kuna ulazima wa kushirikisha wadau wote mara baada ya rasimu ya kwanza
kukamilika ili wadau waipitie kwanza. Alisisitiza rasimu ya pili iwe
imefanyiwa mapitio na kukamilika ifikapo Februari au Machi, 2018 ili
mahitaji ya fedha yaingizwe kwenye mchakato wa Bajeti ya Serikali ya
Mwaka 2018/2019.
Aliwataka
Waheshimiwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta
zinazohusika na mgogoro wa matumizi ya ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo
wafanye ziara ya kutembelea eneo hilo ili wawe na uelewa mpana kuhusu
changamoto za kisekta zilizopo katika eneo husika.
Kikao
hicho kilihudhuriwa na Mawaziri wa Maliasili na Utalii; TAMISEMI; Ardhi
na Maendeleo na Makazi; Naibu Mawaziri wa Kilimo; Maji; Mifugo na Uvuvi
na Elimu na Mafuzo. Pia kilihudhuriwa na wakuu wa taasisi za Serikali,
wawekezaji walioko Loliondo, uongozi wa mkoa wa Arusha, madiwani na
wananchi kutoka Loliondo.
Desemba
2016, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kikazi wilayani Ngorongoro ambako
alipokea taarifa ya kuwepo mgogoro wa matumizi ya ardhi katika Pori
Tengefu la Loliondo. Januari 2017, aliunda Kamati ya Uchunguzi iliyokuwa
na wajumbe 27 ambayo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho
Gambo.
Washiriki
wa kikao hicho waliopata fursa ya kutoa maoni, walipongeza uamuzi wa
Serikali ya awamu ya tano wa kuwashirikisha wananchi hadi ngazi ya chini
katika kutafuta suluhu la mgogoro huo.
Akichangia
kwa niaba ya NGOs, Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya Kiserikali ya
Pastoralist Women Council, Bi. Manda Neritiko aliishukuru Serikali kwa
kuwashirikisha wananchi kutafuta suluhu ya mgogoro huo, hatua ambayo
alisema haijawahi kufanyika miaka yote ya nyuma.
“Huko
nyuma tulikuwa tukipewa maagizo tu, Serikali imeamua hivi, Serikai
imesema vile, lakini kwa awamu hii, tumeweza kuitwa kwenye vikao
mbalimbali na kutoa maoni yetu na hata kupewa mrejesho,” alisema.
Aliomba
hata katika chombo kipya kitakachoundwa, kuwe na uwakilishi wa wananchi
kutoka ngazi ya chini ili waweze kushiriki kikamilifu katika kupanga
namna bora ya kuendeleza eneo hilo.
Kwa
upande wa wawekezaji, Bw. Scott Tineja Mollel kutoka kampuni ya
AndBeyond Tanzania, alisema wao kama wawekezaji wanataka kuhakikishiwa
kuwepo kwa utalii wa kesho. “Hatuwezi kuwa na utalii wa kesho kama
hatutunzi mazingira ya sasa,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni