Jumanne, 26 Desemba 2017

Daktari bingwa feki aliyetibu wagonjwa mwaka mzima anaswa




POLISI mkoani Rukwa inamshikilia mkazi wa kijiji cha Isesa Manispaa ya Sumbawanga, Joseph Pizo (25) kwa kujifanya daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu. Mtu huyo alikuwa akitibu wagonjwa nyumbani kwake bila kuwa na ujuzi wowote wa kitabibu kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, ‘daktari’ huyo alifungua hospitali yake hiyo nyumbani kwake, Isesa Manispaa ya Sumbawanga na kutibu wagonjwa kwa kuwatoza fedha, ambapo wananchi na viongozi wa serikali na wakazi wa kijiji hicho na kwingineko walimiminika na kutibwa na ‘daktari bingwa’ huyo .
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alithibitisha kukamatwa kwa mtu huyo na kusema alikuwa anatoa huduma za udaktari, bila ya kuwa na leseni ya udaktari wala kusomea taaluma huyo.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa saa 4 asubuhi jana, akiendelea kuwahudumia wagonjwa nyumbani kwake na kwamba atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa awali wa shauri lake kukamilika.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mganga Mfawidhi wa Manispaa ya Sumbawanga, Dk Aachie Hellar alieleza kuwa ‘daktari bingwa’ huyo alikamatwa nyumbani kwake, akiwa anaendelea kutibu wagonjwa baada ya taarifa za siri.
Alitaka wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga, kujihadhari na watu kama hao kwa kuwa madhara yake ya baadaye ni mabaya, kwani kitendo hicho kinaweza kusababisha vifo vinavyotokana na usugu wa matumizi yasiyo sahihi ya dawa, lakini pia kusababisha kutokea kwa magonjwa ya ini na figo.
Mfamasia wa Manispaa, Fortunata Kumbakumba ambaye alishiriki kumkamata mtuhumiwa huyo kwa kushirikiana na polisi, alisema kuwa mtu huyo alikuwa akitumia vitabu vya tiba alivyokutwa navyo, kununua dawa na kuwatibu wagonjwa.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo alidai vitabu hivyo vya tiba, alipewa na wazungu waliokuwa wakiishi na kufanya kazi katika Zahanati ya Mumba, inayomilikiwa na Kanisa Katoliki. Baadhi ya wagonjwa waliotibiwa na daktari huyo kwa mashati ya kutoandikwa majina yao, walimsifu kwamba amekuwa akiwatibu vizuri na kupona maradhi yao, yaliyokuwa yakiwasumbua.
Waliiomba serikali imwachie huru, aendelee kuwahudumia wagonjwa. Naye Juddy Ngonyani, Mwandishi wa Kituo cha Azam TV, alikiri kuwa baadhi ya jamaa zake na majirani zake, wametibiwa tiba na daktari huyo, huku wakimsifia kuwa ni daktari mzuri kwani wengi wa waliotibiwa naye wamepona
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni