
Rais
John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa hospitali
ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 23,2017 Kaimu Makamu Mkuu
wa chuo hicho, Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema hospitali hiyo
itakayofunguliwa Jumamosi Novemba 25,2017 imepewa hadhi ya kuwa
hospitali ya rufaa ya Taifa.
Amesema
hilo linatokana na kutoa huduma za kitabibu zinazohitaji madaktari
bingwa na madaktari bingwa wabobezi, huku ikiwa imesheheni vifaa vya
kisasa.
Profesa
Kamuhabwa amesema uwepo wa vifaa vya kisasa na madaktari wa kutosha
utasaidia hospitali kupunguza kwa kiasi kikubwa wagonjwa kwenda nje ya
nchi kupata tiba.
"Hospitali
hii itasaidia kuongeza idadi ya madaktari bingwa kwa kuwa imewekewa
mazingira rafiki kwa ajili ya kufanya uchunguzi na utafiti ili kuboresha
huduma na matibabu," amesema.
Amesema
ujenzi wa hospitali hiyo ni mwendelezo wa Kampasi ya Mloganzila ikiwa
ni jitihada za Serikali katika kuboresha chuo hicho.
Naibu
makamu mkuu wa chuo na mwangalizi wa huduma za hospitali, Profesa Said
Abood amesema hospitali hiyo ina mfumo wa Tehama katika kutuma na
kupokea sampuli hivyo kurahisisha kasi ya majibu na huduma.
Amesema
huduma zote za hospitali zipo katika jengo moja, hivyo hakutakuwa na
usumbufu wa mgonjwa kuzunguka kufuata utaratibu ili kupata matibabu.
"Tuna
vifaa vya kisasa ambavyo ni vichache nchini au havipo kabisa, mfano
kifaa cha kuvunja mawe kwenye figo bila upasuaji," amesema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni