Rais
John Magufuli amemteua aliyekuwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah
kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, huku aliyekuwa Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu akiteuliwa kuwa balozi.
Dk
Kashilillah ameteuliwa ikiwa ni takriban wiki tatu kupita tangu
alipoondolewa katika wadhifa wa Katibu wa Bunge, nafasi iliyochukuliwa
na Stephen Kigaigai.
Rais Magufuli Mei 28,2017 alitengua uteuzi wa IGP Mangu na kumteua Simon Sirro kushika wadhifa huo.
Mangu anasubiri kupangiwa kituo cha kazi pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Dk Aziz Mlima.
Uteuzi
wa Rais Magufuli, uliotangazwa Alhamisi Oktoba 26,2017 na Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi John Kijazi uliwahusu pia, makatibu wakuu, naibu
makatibu wakuu na wakuu wa mikoa ambao wataapishwa Ijumaa Oktoba
27,2017 mchana Ikulu jijini Dar es Salaam.
Balozi
Kijazi amesema Rais Magufuli amewateua naibu makatibu wakuu wapya saba
na kuwapandisha naibu makatibu wakuu wanne kuwa makatibu wakuu kwenye
baadhi ya wizara.
Pia, amewahamisha makatibu wakuu wanne na naibu katibu mkuu mmoja kwenda kwenye wizara nyingine.
Balozi
Kijazi amesema katika nafasi za wakuu wa mikoa, Rais Magufuli amewateua
wa mikoa sita, miongoni mwao ni aliyewahi kuwa waziri katika utawala
uliopita wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Adam Malima anayekwenda Mkoa wa
Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti amepandishwa cheo na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Balozi
Kijazi amesema wakuu wa mikoa walioondolewa kutokana na kustaafu ni
Joel Bendera (Manyara), Meja Jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga (Geita) na
Kamishna Msaidizi Mwandamizi mstaafu wa Polisi, Zelothe Stephen (Rukwa).
Wakuu wa mikoa walioachwa ni wa Mtwara, Halima Dendego, Jordan Rugimbana (Dodoma) na Dk Charles Mlingwa (Mara).
Amesema
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Joackim Wagambo ameteuliwa kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Rukwa, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel amekuwa Mkuu wa
Mkoa wa Geita na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme akiwa mkuu
wa mkoa huo.
Galesius Byakanwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni