Jumatatu, 2 Oktoba 2017

Mnyarwanda jino kwa jino na Okwi


 STRAIKA wa Singida United, Mnyarwanda, Danny Usengimana, amesema ndiyo ameanza kazi ya kufunga na ataendelea kufanya hivyo ili kufikia lengo lake la kuwa mfungaji bora msimu huu.

Usengimana aliyejiunga na Singida msimu huu akitokea Polisi ya Rwanda, mpaka sasa amefanikiwa kucheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara kati ya tano ambazo timu yake imeshacheza na kufanikiwa kufunga bao moja.

Mnyarwanda huyo alikosa mechi tatu za mwanzo kutokana na kuwa majeruhi. Juzi Jumamosi alifunga bao moja kwenye mchezo dhidi ya Azam uliopigwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na kutoka sare ya bao 1-1.

Kutokana na kauli hiyo, ni wazi Mnyarwanda huyo ameingia vitani na straika wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi ya kuwania Tuzo ya Ufungaji Bora kwani kwa sasa Okwi anaongoza akiwa na mabao sita kabla ya mchezo wao wa jana Jumapili dhidi ya Stand United.

“Namshukuru Mungu kwa kunijalia, nimefunga bao langu la kwanza katika ligi hii, nitaendelea kupambana na nitazidi kumuomba Mungu azidi kunifanya niwe na afya njema ili niweze kufikia malengo yangu.

“Nataka kuwa mfungaji bora kama nilivyofanya kule nilipotoka, hivyo mwanzo huu wa kufunga kwangu unanipa faraja,” alisema Usengimana ambaye kabla ya kutua Singida United, alikuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Rwanda kwa misimu miwili mfululizo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni