
Almasi
zenye uzito wa kilogramu 29.5 za thamani ya zaidi ya Sh bilioni 64,
ambazo zilibakiza dakika tano tu kutoroshwa kutoka katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (JNIA) kwenda ughaibuni, zimetaifi
shwa na serikali.
Aidha,
watumishi wa serikali na maofisa wa Mgodi wa Almasi wa Williamson wa
Mwadui Shinyanga, waliohusika na uthaminishaji wa awali wa almasi hizo
na kudanganya kuwa zilikuwa na uzito wa kilogramu 14 tu, watachunguzwa
na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Hayo
yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip
Mpango alipokuwa akipokea ripoti ya timu ya wataalamu, iliyoundwa
kuchunguza upya uzito na thamani halisi ya almasi hizo baada ya
kuzikamata katika uwanja huo wa JNIA Agosti 31, mwaka huu.
Uthamini
uliofanywa awali kwa almasi hiyo, iliyokuwa mbioni kupakiwa ndani ya
ndege kutoroshewa nchini Ubelgiji, ulieleza kuwa ilikuwa na thamani ya
chini ya Sh bilioni 32, huku ikielezwa pia kuwa na kilogramu 14, taarifa
zilizogundulika kuwa zilikuwa ni za uongo.
Jana
Waziri Mpango alipokea maelezo ya almasi hiyo kutoka kwa Kiongozi wa
Jopo la Wataalamu waliofanya uthamini mpya, Profesa Abdulkarim Mruma na
wasaidizi wake.
Baada
ya kuridhika na maelezo, yaliyodhihirisha kuwepo kwa kiwango cha juu
cha udanganyifu kuhusu uzito na gharama za almasi hiyo, kwa lengo la
kuliibia taifa, Waziri Mpango aliagiza almasi hiyo yote kutaifishwa,
kupigwa mnada na fedha zitakazopatikana kuingia serikalini.
Aliagiza
pia kuwajibishwa kwa maofisa wa serikali waliohusika katika udanganyifu
huo kwa wahusika hao kukamatwa, kuchunguzwa mali zao ikiwemo majumba,
mashamba, magari kuona kama vinaendana na mishahara yao na baadaye
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Alisema,
Watanzania wamechoshwa kuona mali zao zikiibiwa kila kukicha huku
serikali ikikosa mapato makubwa kutokea katika rasilimali hizo.
Pia,
aliagiza kuandaliwa kwa wataalamu wa madini na wapelekwe kwenye migodi
haraka, kukabiliana na wizi wa aina hiyo, huku akivitaka vyombo vya
ulinzi na usalama kukabiliana na wizi wa aina hiyo.
Waziri
Mpango aliagiza pia upimaji wa madini kufanyikia kwenye eneo la migodi,
na pia kununuliwa kwa mashine za kupimia madini kwenye maeneo ya
migodi, baada ya kuelezwa na Profesa Mruma kuwa ukosefu wa vifaa vya
kupimia ni chanzo cha udanganyifu huo.
“Kazi
nzuri sana umefanya Professa Mruma na wenzako na kwa sasa ninaagiza
haya madini tuliyokamata hapa, kulindwa kuanzia hapa hadi pale
yatakapoingizwa sokoni, pia ninamtaka Gavana wa Benki Kuu (Profesa Benno
Ndulu) kuanza kuhifadhi madini ya vito na si fedha peke yake.
“Inashangaza
kuona maofisa wa juu wa Wizara ya Nishati na Madini waliokuwa na jukumu
la kuthaminisha madini haya wamedanganya huku wale walio chini yao
wametoa tathmini ya kweli, sasa huu ndiyo uzalendo unaotakiwa,”
aliongeza Dk Mpango.
Kwa
upande wa Mgodi wa Williamson Diamond LTD, Waziri Mpango alisema
kutokana na kubainika kujihusisha na udanganyifu, huku kampuni hiyo
ikieleza kupata hasara kila mwaka, kuanzia mwaka huu itawajibika kutoa
gawio serikalini na alimuagiza Profesa Mruma kuijulisha Bodi ya Kampuni
hiyo agizo hilo la serikali mara moja.
Kwa
upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salam, Lazaro
Mambosasa akizungumzia agizo hilo, alisema kuwa hakuna mtuhumiwa ambaye
hatoshughulikiwa katika kosa hilo.
Alisema
sheria itafuata mkondo na kuwa kila mtu ambaye ameshiriki kwa namna
moja au nyingine, atakamatwa kuanzia wale waliopo mgodini hadi wale
walioshiriki katika kutaka kutorosha madini hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni