Ingawa vita vya miaka mitatu vya Mosul nchini Iraq vinakaribia kuisha, makovu ya mateso ya kimwili na kiakili walioachiwa watoto yatachukua muda kupona. Taarifa kamili na Flora Nducha.
(Taarifa ya Flora)
Hayo ni kwa mujibu wa Naibu Mwakilishi wa UNICEF nchini Iraq Bi. Hamida Ramadhani, ambaye amesema katika siku tatu zilizopita shirika lake na wadau wengine wameshuhudia ongezeko la watoto walio katika hali ya hatari wakiwasili peke yao katika vituo vya afya na maeneo ya upokeaji, na wengine wachanga wakiletwa baada ya kuokolewa wakiwa pekee yao katika vifusi.
Amesema wasichana kwa wavulana takriban 650,000 walioishi katika jinamizi la vita wamelipa gharama kubwa wakivumilia vitisho na unyanyasaji wakati wa mapigano makali ya miezi kumi na bado kuna wengine wanaoendelea kuteseka na mapigano yanayoendelea katika baadhi ya maeneo Magharibi mwa Mosul.
Kwa mantiki hiyo UNICEF inasisitiza wito wake kwa pande zote katika vita nchini Iraq kuwatendea haki watoto wote, ikisema sasa ndio wakati wa kuwaokoa, kuondokana na maumivu, kuungana tena na familia zao na kuwarejesha tena kufurahia utoto wao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni