Tahadhari iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO imesema ukosefu wa mvua Afrika Mashariki umeongeza njaa zaidi na kusababisha mazao kuteketea, lishe kupungua na maelfu ya mifugo kufa, wafugaji wakibeba mzigo mkubwa wa ukosefu huo wa mvua.
Tahadhari hiyo imeonya kwamba mfululizo wa tatu wa ukosefu wa msimu wa mvua umeathiri zaidi Somalia kusini na kati, kusini mashariki mwa Ethiopia, kaskazini na Mashariki mwa Kenya, Kaskazini mwa Tanzania pamoja na kaskazini mashariki na magharibi mwa Uganda, ambako watu wamepoteza ujasiri wao na kukosa mbadala wa kukabiliana na baa hili.
FAO imesema idadi ya watu wanaohitaji msaada wa dharura wa kibinadamu katika maeneo hayo tajwa, ambayo sasa inakadiriwa kuwa milioni 16, imeongezeka kwa asilimia 30 tangu mwishoni mwa mwaka 2016 na iwapo msaada wa haraka hautatolewa basi hali yao itakuwa mbaya zaidi kwani msimu wa kiangazi unawadia katika miezi michache ijayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni