Wakati
Kampuni ya Acacia ikisema imepoteza mapato ya Sh385 bilioni katika
kipindi cha miezi sita kutokana na kuzuiwa kusafirisha mchanga wa madini
nje, Rais John Magufuli ametishia kufunga migodi ya wawekezaji iwapo
hawatajitokeza mapema katika mazungumzo.
Rais
Magufuli amesema hayo takriban wiki moja baada ya kudokeza kuwa
Serikali ingeanza mazungumzo “na waliokuwa wanatuibia” mapema wiki hii.
Jana,
Rais Magufuli alisema Serikali haitasita kufunga migodi yote ya madini
ambayo wamiliki walitakiwa kufanya mazungumzo na Serikali kuhusu ulipaji
kodi.
Akizungumza
katika ziara yake mkoani Kigoma ambako alizindua Barabara ya
Kibondo-Nyakanazi, Rais Magufuli alisema Taifa linapoteza fedha nyingi
kutokana na upotevu wa madini.
“Ni
matrilioni ya fedha ambayo yanapotea, na sasa hivi tumewaita tufanye
mazungumzo lakini wakichelewachelewa nitafunga migodi yote,” alisema.
Alisema ni bora migodi hiyo ikakabidhiwa kwa Watanzania kuliko wawekezaji ambao hawalipi kodi.
Rais
Magafuli alipiga marufuku usafirishaji wa mchanga huo nje ya nchi, na
baadaye kuunda kamati mbili; moja ya kuchunguza kiwango cha madini
kilichokuwa katika makontena 277 yaliyozuiwa Bandari ya Dar es Salaam na
nyingine kuangalia athari za kiuchumi na kisheria tangu mchanga huo
uanze kusafirishwa mwaka 1998.
Ripoti
ya kamati ya kwanza ilisema kuwa Acacia, inayoendesha migodi ya
Bulyanhulu na Buzwagi, haikusema ukweli kuhusu kiwango cha dhahabu,
ikidai kuwa imebaini mchanga huo una madini hayo mara kumi ya kiwango
kilichotangazwa na wawekezaji hao.
Ripoti
ya kamati ya pili ilionyesha kuwa katika kipindi cha miaka 20, Serikali
ilipoteza zaidi ya Sh108 trilioni na kwamba Acacia haijasajiliwa nchini
na hivyo inafanya kazi kinyume cha sheria.
Hata
hivyo, Acacia haijakubaliana na matokeo ya ripoti hizo, ikisema inataka
uchunguzi wa kamati huru na kwamba kama matokeo hayo ni ya kweli,
Tanzania ingekuwa moja ya nchi tatu zinazozalisha dhahabu kwa wingi
duniani.
Jana,
Acacia ilisema imepoteza Sh385 bilioni katika kipindi cha miezi sita.
Acacia pia imesema endapo hali itaendelea kuwa hivyo, italazimika
kuufunga mgodi wake wa Bulyanhulu na kusitisha mikataba ya ajira kwa
wafanyakazi.
Hata
hivyo, katika taarifa yake ya jana inayozungumzia kipindi cha Januari
mpaka Juni, Acacia imesema imepata changamoto kubwa katika utendaji
wake nchini.
“Nusu
(ya kwanza), imetupa changamoto kubwa katika shughuli zetu Tanzania
baada ya kuwekewa zuio la usafirishaji wa makinikia kuanzia Machi,”
alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia, Brad Gordon. “Mapato yetu
yameshuka mpaka dola 175 milioni za Kimarekani kutoka dola 318 milioni
tulizotarajia.”
Licha
ya kushindwa kuingiza Dola 175 milioni za Marekani (zaidi ya Sh385
bilioni) zilizotarajiwa, Acacia inasema imelipa dola51 milioni za Kodi
ya Ongezeko la Thamani (VAT), ambazo ni zaidi ya Sh112.2 bilioni.
Ili
kulinda masilahi ya wanahisa wake, Acacia imewasilisha notisi kwa
msuluhishi kwa ajili ya migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi ambayo ndiyo
inayozalisha mchanga wa madini kwa sasa.
Buzwagi
imekuwa ikisafirisha mchanga huo kwenda nje ya nchi kwa ajili ya
kuuyeyusha ili kupata mabaki ya dhahabu, shaba na fedha kutokana na
teknolojia hiyo kutokuwapo mgodini.
Hatua
ya kwanza ya kuchenjua dhahabu hufanyika mgodini na mchanga unaosalia
ndio unaosafirishwa nje. Acacia imekuwa ikieleza kuwa mchanga huo una
asilimia 0.02 ya dhahabu wakati shaba ni asilimia 10.
Acacia pia imekanusha taarifa ya kuwapo amri ya kutakiwa kuondoka nchini kwa mmoja wa wafanyakazi wake wa kigeni.
“Hatuna
taarifa za kutolewa kwa amri hiyo kwa mfanyakazi wetu yeyote wa kigeni
aliyepo Tanzania. Tunashirikiana vizuri na Serikali kwenye mazungumzo
yanayoendelea na hakuna aliyekamatwa habari hiyo si sahihi,” inasema
taarifa hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni