ziara ya Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi kwenye jimbo lake umekua na neema katika kata za Idete na Fumo baada ya mbunge huyo kuchangia Sh Milioni Sita kwenye ujenzi wa Kituo cha Afya, Zahanati, Miundombinu ya Barabara na ujenzi wa Hosteli ya Sekondari Matundu Hill.
Akizungumza katika kata ya Idete ambayo wananchi wake walimueleza changamoto yao ya ujenzi wa kituo cha afya na hostel ya shule hiyo Mbunge huyo aliahidi kutoa Sh Milioni 2.8 kwenye kata hiyo ili ielekezwe kwenye ununuzi wa mifuko 50 kwa ajili ya kituo cha afya na mifuko mingine 50 ya ujenzi wa hostel hiyo huku akitoa Sh Laki Tatu ili inunue Projector ya kufundishia shuleni hapo.
Mbunge Kunambi amesema anafahamu umuhimu wa elimu ni mkubwa na yeye kama kiongozi ambaye anaunga mkono juhudi za serikali ya Rais Dk John Magufuli ya kutoa elimu bila malipo ana wajibu wa kuchangia ujenzi huo ili kuendelea kuzalisha kizazi cha wasomi nchini.
" Wakati wa kampeni nilipita na mkanieleza shida zenu, nimekuja hapa ili tuanze na zile changamoto kubwa kwetu lakini lengo letu ni ndani ya miaka mitano hii mliyotupa dhamana kuhakikisha tunakamilisha kwa kiasi kikubwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama ambavyo ilituelekeza," Amesema Mbunge Kunambi akiwa katika kata ya Idete.
Amesema hii ni ziara yake ya kwanza tangu aapishwe kuwa Mbunge na mpaka sasa ameshatembelea kata 11 kati ya 16 zilizopo kwenye jimbo lake huku akitatua changamoto mbalimbali kwenye kata zote alizozitembelea.
" Ziara yangu ina sura mbili moja ni kuwashukuru kwa kumchagua kwa kishindo Rais wetu Dk Magufuli, mimi mbunge wenu na madiwani wa CCM, tulianzia Kata ya Uchindile na bado tuna kata tano ili tuhitimishe kata zote 16, lakini sura ya pili ni kuanza kutatua changamoto na kero zetu, niwaahidi zipo ambazo tutazimaliza ndani ya mwezi mmoja, zipo tutakazochukua mwaka mzima na zipo ambazo tutazimaliza ndani ya miaka mitano, lakini niwahakikishie hatutoacha sehemu," Amesema Mbunge Kunambi.
Akiwa katika kata ya Fomu, Kunambi pia amechangia Sh Milioni 3.5 ili zielekezwe kwenye kumalizia boma la ujenzi wa kituo cha afya pamoja na kusaidia kivuko cha awali kwenye barabara ya kata hiyo ili wananchi waweze kupata bila kupata shida.
Akizungumza baada ya mchango ya mbunge huyo mmoja wa wanufaikaji ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya matundu Hills Kasmiri Stephano amempongeza Mbunge huyo kwa jitihada zake hizo huku akisema zitasaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi hasa wa kike ambao watakua wakikaa kwenye hostel hizo huku akimuomba kuzidi kuiangalie shule hiyo.
" Namshukuru sana Mbunge wetu, kumalizia ujenzi wa hostel yetu kutakua ni msaada kwetu sisi wanafunzi wa kike lakini pia ametoa fedha za kununulia projector kitu ambacho tunaamini kitakua ni msaada kwa walimu wetu katika kutufundishia," Amesema mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo.